LATEST POSTS

Wednesday, September 16, 2015

MJUE SAIDI TUMBA SAID KANDA TOKA SUPER MATIMILA HADI BENDI YAKE HUKO UINGEREZA.



                   MJUE MWANAMUZIKI SAIDI TUMBA SAIDI                                                 KANDA.
                                                               SAIDI TUMBA.

 Leo mgeni wetu katika Kavasha si mwingine bali ni Saidi Kanda,maarufu Saidi Tumba ambae ni Mtanzania aishie na kufanya kazi Jijini London Uingereza.






                                      SAIDI KANDA AKIWA NA MONGO REY.

Saidi Tumba alizaliwa katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani,Alianza kazi ya muziki tangu akiwa shuleni katika shule ya Msingi Mwambao mjini Bagamoyo,mwanzoni mwa miaka ya 1970 ambapo mnamo mwaka 1975 alianzisha kikundi cha ngoma Shuleni hapo,na kila Jumamosi alikua akienda kupiga ngoma katika kundi moja lililojulikana kama Kizibo Band hadi alipomaliza shule alikua akifanya hivyo.
 
                               AKIWA NA CHAMPION DRUMMER WA KOFFI OLOMIDE

Baada ya kumaliza Shule hakuendelea na elimu ya Sekondari ndipo Mjomba wake Abdu Hassan Mpitu’’Chamcho’’aliekuwa  akifanya kazi katika Bendi ya Biashara Jazz alipomchukua na kuungana nae katika Bendi hiyo ambayo ilikua ikiongozwa na Juma Ubao’’ King Makusa’’ambapo alidumu hadi Mwanzoni mwa  1980 alipojiunga na Remmy Ongala katika Bendi ya Super Matimila ambapo ni mpiga gitaa Battie Ossenga aliemchukua kutoka Biashara Jazz na kujiunga na Bendi hiyo.
                      AKIWA NA ORCHESTRA SUPER MATIMILA MWAKA 1989

Kati ya mwishoni mwa Mwaka 1987 na mwanzoni mwa 1988 alichukuliwa na Nguza Viking kwenda kwenye kampuni ya Orchestra Maquis Company iliyojulikana kwa ufupi OMACO ambapo alikaa kwa muda mfupi wa miezi 6 kabla ya kurudi Super Matimila ambapo mwaka huo mwishoni walifanya ziara Ulaya ambapo mwaka 1989 aliamua kuachana na Bendi hiyo na kuanza maisha Nchini Uingereza ambapo pamoja na wakongo waishio Nchini Uingereza walianzisha Bendi iliyoitwa Banoma ikiwa na wanamuziki kama Fiston Lusambo,Koko Anana,Lisalisa na wengineo akiwemo Suleiman Mbwembwe huyu aliekuwa Vijana Jazz na baadae Msondo Ngoma.
                             SAIDI KANDA NA MVULAMANDONDO BAND.

Wakati mwingine alifanya Zingzong na wanamuziki kama Papa Wemba, Reddy Amis,Stino Mubi,Diesy Mkangi Adole,Mongo Ley,Burkina Fasso Nk,Pia hufanya kazi za aina hiyo na Mpiga muziki wa Jazz Maarufu nchini Uingereza Alan Skidimore na Mwanamuziki wa Marekani aitwae Grace Jones,kundi letu rasmi la Zingzong huitwa Zingzong  All Stars ambapo tupo wanamuziki 9 na linaongozwa na Fiston Lusambo na hivi karibuni walirekodi katika Studio za Ketebul,Nairobi Nchini Kenya akiwa na Nzaya Nzayadio Na Fiston.
 
             AKIWA STUDIO ZA KETEBUL JIJINI NAIROBI MWAKA HUU.

Kwa hivi sasa anafanya kazi katika Bendi yake mwenyewe ijulikanayo kama Mvulamandondo ambayo baadhi ya kazi zake ameziweka katika mtandao ambao utauona baadae,huwa anapiga na wanamuziki wa zamani Mfano Nzaya Nzayadio aliekuwa Orchestra Lipualipua,Bendi hii anasema imempa umaarufu na mafanikio makubwa nchini Uingereza  na pia amefundisha watu wengi sana kupiga ngoma nchini humo kitu kilichomfanya kuwa na jina kubwa Uingereza na kujulikana kama mpiga ngoma mkubwa ingawa watu wengi hudhani kuwa si Mtanzania kwa kuwa hufanya kazi na watu wa Afrika Magharibi.
            SAID KANDA AKIWA NA NZAYA NZAYADIO WA ILIYOKUA LIPUA LIPUA

Muziki wa Tanzania kwa kweli bado unapendwa Barani Ulaya kwani hupigwa sana katika matamasha mbalimbali utasikia muziki wa Tanzania ingawa kwa ndani ya Tanzania muziki wa dansi umeshuka kutokana na kuandaliwa kistudio zaidi na sio kwa kupiga zana kihalisia ingawa kwa upande wa masoko promosheni ipo juu ingawa muziki wenyewe upo chini sana haujiuzi kulinganisha na wakati wa nyuma ambapo muziki ulikua ukijiuza wenyewe na promosheni ilikua chini mno. Kwa Kweli Dokta Remmy Ongala alifungua njia ya kuutangaza muziki wa Tanzania barani Ulaya kazi kwetu kuendeleza kazi hiyo nzuri ya Dokta Remmy.
                             BENDI YA DOKTA REMMY SUPER MATIMILA.

Kazi Ulaya huwa kimfumo zaidi na nilazima uwe na Meneja na wakala na tuna kazi nyingi sana toka kwa ajenti wamuziki na kazi zetu zinapendwa sana ndio maana hata Bendi yangu ya Mvulamandondo ipo imara hadi leo nikipiga Rhumba na muziki wa asili anasema Saidi Tumba,Aliongeza kuwa katika kundi lake la Zingzong  la All Stars Mtanzania peke yake,Lakini  anasema katika Bendi yake yupo Mtazania mmoja aitwae Fabby Moses,anaongeza kuwa kwa Nchini Tanzania anavutiwa sana na Ally Kiba na anamshauri ajikite kwenye kuwa na Bendi kwani anakipaji kikubwa.
                                                  KIKOSI CHA SUPER ZINGZONG.

Saidi Tumba anahamu ya kurudi nyumbani sasa baada ya kukaa nje kwa zaidi ya miaka 26.Anawashauri  Watanzania kuacha kuwa tofauti na walivyo katika muziki,wawe halisi na sio kwa kuiga watu,pia wasipende kutumia playback na kupiga muziki kwa midundo ya kutengeneza studio badala yake wanamuziki hasa wa kizazi kipya  wajifunza zana za muziki kama Ngoma,Kinanda,Guitar nk.
                         BENDI YA SAIDI KANDA IITWAYO MVULAMANDONDO

Miziki ya asili ya makabila ya nyumbani ni muhimu na mimi huwa napiga sana hiyo kwani nina elimu na miziki ya asili hata zana za muziki za asili hutengeneza mwenyewe kama vile gitaa la dungu na zeze pia,alimaliza Saidi Tumba.
                         SAIDI KANDA NA GITAA LAKE LA KIASILI  ''DUNGU''

                   Saidi Kanda Tumba anapatikana kwa mawasiliano yafuatayo
                                     Simu namba +447404066607
                               Website-www.mvulamandondo.com
                                       Pia-www.saidikanda.com
                                  
                                   PICHA ZAIDI ZA SAIDI KANDA

 
                                              AKIWA NA KANDA BONGO MAN.
 
                                      AKIWA NA CHRISS JONES ZINGZONG ALLSTARS
 
                                                  ZING ZONG ALL STARS BAND
 

                                                                CHRISS JONES
 
                                              SAIDI NA ADORE WA ORCHESTRA KIAM 









0 comments:

Post a Comment