MASHUJAA BAND YAPAGAWISHA WAKAZI WA LINDI HAPO JANA SEPT 12-2015.
Siku ya Jumamosi 12 Septemba 2015,Bendi ya Mashujaa ilifanya
onesho la kufana katika Hotel ya Peace Beach Mjini Lindi na kuhudhuriwa na
mamia ya wakazi wa Mjini humu.
Kwa ufupi mambo yalikua kama hivi-Saa 21:30 Wapiga ala
wakiongozwa na Baba Isaya na Freddy Masimango walianza kupasha ala zao moto
hadi pale Saa 22:30 Raja Ladha alipokuja kuendeleza harakati kwa machombezo
anuwai hadi saa 23:05 pale Mirinda Nyeusi alipofika kuongezea yake ambapo
aliweka hadharani nyimbo mpya mbili zenye utamu wa aina yake Mama wa Kambo na
Magdalena ambao una midundo flani amazing ya kiasili ambao ulionekana kuwakuna
mashabiki vilivyo.
Mambo yalikua tele ama kwa hakika kwani muda si mrefu majira
ya Saa 23:20 Kundi la wasanii wa Bongo Movie likiongozwa na Mwenyekiti wa
‘’Mama Sema na mwanao’’ Steven Mengele ‘’Steve Nyerere maarufu kama Tajiri
Mfupi ama Tajiri mbishi nao walitinga maeneo ya kiota hicho cha burudani wakiwa
pamoja na Odama,Wastara,Maya,Chuchu Hansi
nk amabao waliungana na Wema Sepetu na Petit Man Wakuache ambao
waliingia mapema zaidi.
Chombezo linaendelea ambapo Patient Buddas anapanda jukwaani
kuungana na Raja Ladha na kutelemsha kitu murua ambacho ni kopi ya Werrason
Ngiama Makanda hadi pale saa 23:50 amabapo programu ya Bendi inaanza rasmi
Charz Baba,Jado FFU wanaingia na kushusha vibao mfululizo wakianza na Mama
Kibonge,Safari yenye vikwazo,Deodata ambao Raja Ladha aliutendea haki hasa na
katika wimbo huo ndipo timu ya wacheza show ilipoibuka na kuongeza shangwe kwa
mashabiki ambao hawakutaka kabisa kukatizwa kwa Sebene wao walitaka ‘’kuchinja
bata tu’’
Kuanzia Saa 01:30 kwa Nusu saa nzima aliamua kuwapagawisha
mashabiki kwa machombezo mseto ya baikoko na Mchiriku ambapo vipande vya
naipenda Simba na Naipenda Yanga mshabiki wa damu viliwapagawisha mashabiki wa
timu husika pale inapotajwa timu yao ambao mambo ya dau la Mtani Jembe
yalionekana kuchukua nafasi hadi pale alipowatuliza kwa Wimbo wake maarufu wa
Risasi Kidole ambapo Rapa Bora mara nyingi mfululizo Saulo Fergusson nae
aliibuka kuja kufanya yake,ikafata Mama mimi nashangaa wimbo utunzi wa Mirinda
Nyeusi ambalo ni Rhumba la ukweli.
Saa 02:30 Steve Nyerere anakaribishwa kwa nyakati tofauti
pamoja nae Wastara kuja kusalimia kisanii ambapo alijaribu kupita walipopita
mastaa mwisho akatoka nje kidogo ya mstari pale alipotoa za aliselema kitu
kilichoibua mitizamo ya kiitikadi ambapo kwa haraka Meneja wa Bendi ya Mashujaa
Martin Sospeter aliwahi kurekebisha na programu ikaendelea hadi mwisho.
TATHMINI YA ONYESHO
1.MAHUDHURIO-Ilianza kwa uchache lakini kufika katikati ya
onesho Ukumbi ulijaa sana.
2.HALI YA JUKWAA-Iliathiri ufatiliaji kwa wahudhuriaji
walioketi kwani hawakuweza kuona mbele pale wenzao wanapoamka na kwenda kucheza
kwani eneo la jukwaa limeinuliwa kwa sentimeta chache sana kutoka chini.
3.NISHATI YA UMEME- Hali ya kuungua na kuongezeka kwa umeme
ilionekana kuwa tishio kwa onesho kama sio juhudi za wahusika wa Bendi na
Hoteli wa kutumia jenereta moja kwa moja bila kujali uwepo wa umeme.
4.HALI YA BENDI-Bendi ilikua katika hali nzuri na walikua
katika morali ya kufanya kazi ingawa baadhi ya waliohudhuri walihoji kutokuwepo
kwa Nguli Elistone Angai ambapo inasemwa ataungana na wenzake leo katika onesho
lao la pili katika Wilaya ya Nachingwea,Mwingine ambae hakuwepo ni Rapa Sauti
ya Radi ambae haijajulikana anamatatizo gani.
5.NYOTA WA ONESHO-Karibia wote walijitahidi kwa kadiri ya
uwezo wao,ala zilikung’utwa vizuri ila Kinanda cha Freddy kilikua habari ya
show,aidha Charz Baba,Mirinda na Raja Ladha ilikua siku yao.
6.UMALIZIAJI WA ONESHO-Kabla ya wimbo wa Mwisho nadhani
hakukuwa na mawasiliano mazuri kwani baadhi ya wapigaji walikwisha weka vifaa
chini na hata ulipoongozwa wimbo huo haikuwezekana na huo ndio ukawa mwisho wa
show hiyo.
Wito- kuwe na mawasiliano mazuri katika kumalizia show kwani
kunawafanya watu waondoke na hamu yao kulikoni kuwaondoa na sintofahamu kama
ilivyokua.Kwa asilimia 95% show ilikua nzuri sana kulinganisha na maonesho
kadhaa ya Mashujaa ambayo nimepata kuyahudhuria na hata kwa maoni ya wengine
waliohudhuria akiwepo mmiliki wa duka la Hadjis Fashion Ndugu Hadji Chaula
ambae amesema onesho hilo ni la ukweli kuliko lile lililofanyika awali Mjini
hapa.
TAKE HOME-Meneja wa Bendi hiyo Ndugu Martin Sospeter
amedokeza kuwa Bendi hiyo itaweka kambi kwa muda wa wiki mbili Mjini hapa kwa
ajili ya maandalizi ya vibao vyao vipya vinavyotarajiwa kuwa moto wa kuotea
mbali.
KILA LA HERI WAZEE WA KIBEGA MASHUJAA BAND.
0 comments:
Post a Comment