LATEST POSTS

Tuesday, February 23, 2016

MAHOJIANO KATI YA KAVASHA GROUP NA M-TANZANIA ,JAZZ PIANIST/AUTHOR, LISTER ELIA.

Leo tuna mgeni ambaye ni mtanzania aishiye na kufanya kazi mashariki ya mbali kule nchini Japani,si mwingine bali ni ndugu yetu Lister Elia ambaye anafahamika sana kwa uhodari wake wa upapasaji wa kinanda,Kavasha ilifanya nae mazungumzo na ilikuwa kama ifuatavyo;                
                                                           Ndugu   Lister  Elia.

1.Habari yako kaka Lister,watanzania na wote wasomao blog yetu ya Kavasha wangependa kujua historia yako japo kwa kifupi.

Lister anajibu;Nashukuru kwa kunikaribisha katika jamvi hili tukufu la KAVASHA,kitaaluma mimi ni Pianist/Keyboardist na pia ni mwandishi wa vitabu,hadi sasa nimeandika vitabu vitatu ambavyo ni 1.Jifunze Gitaa,2.Jifunze Piano na ‘’The mystery of Tamko’s death" ambacho ni cha riwaya.

Nilisomea masomo ya awali ya muziki kule Bukoba katikachuo kiitwacho Ruhija Musical Academy,elimu ya kati ya muziki kule Vienna Austria na elimu ya juu ya muziki nimesomea katika chuo kiitwacho Mate School of Music kilichopo Jijini Tokyo Japani.
Pamoja na kupiga muziki kama mwanamuziki wa kulipwa,lakini pia nafundisha muziki katika vyuo mbalimbali vya muziki Japani kama njia nyingine ya kujiongezea kipato,nilianza kupiga kinanda tangu nikiwa na umri wa miaka 6 kwani kinanda kilikuwa kwenye anga zangu wakati wote kwa nia kujifurahisha tu na sikujua kama ndiyo itakua shughuli yangu kuu siku za baadae kama ilivyo sasa.

Wasifu wangu na mengine mengi yanapatikana kwenye tovuti yangu ambayo ni www.listerelia.com

2.Kavasha ikamuuliza ni lini alianza kujishughulisha na shughuli za muziki?

Lister anajibu;Shukrani za kipekee zimfikie Kikumbi Mwanza Mpango ‘’King Kikii’’,yeye ndiye aliyenishawishi kupiga dansi katika bendi yake kwa mara ya kwanza katika Bendi yake ya King Kiki Double O Orchestra,Baadae nilikuwa kiongozi wa bendi iitwayo Benebene Group,tulipiga zaidi katika mahoteli ya kitalii... zaidi tukipiga katika Hotel ya Kilimanjaro ukumbi wa Tanzania Room kama uwanja wa nyumbani.
                                     Mzee Kikumbi Mwanza Mpango-King Kik

Bendi yangu ya tatu ilikuwa Sambulumaa ambapo nilipiga nyimbo kama Kadiri mke wangu na CCM imekua zilizotikisa sana anga la muziki wa dansi miaka hiyo’’sikiliza nyimbo hizo katika….. https://youtu.be/JPvLxCSeLIU na https://youtu.be/p7DihqWrr8

Bendi yangu ya nne ilikuwa OSS Ndekule na ya mwisho nchini Tanzania kabla sijaelekea nje ya nchi ni bendi ya MK Group maarufu kama wana’’ Ngoma za Maghorofani’’,hapo nilipiga na kurekodi nyimbo lukuki mojawapo ni Maumivu Makali utunzi wa marehemu Joseph Bartholomew Mulenga ipo hapa https://youtu.be/4gbuerY3Fv4

3.Je Uliondoka lini na ulianza anzaje muziki ughaibuni?

Lister anajibu;Niliondoka Tanzania mwaka 1991 nikiwa na mipango ya kwenda Paris,Ufaransa kufanya kazi kama mwanamuziki wa kulipwa,mdhamini wetu alikuwa mwanamke Mfaransa mwenye asili ya Israel ambae aliamua tupige kambi jijini Nairobi Kenya kabla ya kuelekea Ufaransa.Nikiwa hapo Nairobi,safari ya kuelekea Japan ilijitokeza kwanza hivyo,nilibadili mawazo na kuelekea Mashariki ya mbali badala ya kwenda Ulaya.


                                         Lister akiwa safarini kikazi na wenzake.

4.Ni wanamuziki gani na bendi gani ambazo ulifanya nazo kazi huko nje ya Nchi?

Lister anajibu;Nimefanya kazi na wanamuziki wengi wa kimataifa toka nchi mbalimbali,majina ni mengi mno na bendi ni nyingi mno ila,la muhimu ni kwamba pamoja na kupiga miziki ya kwetu na ya wengine,ninalo kundi langu,tunapiga Jazz music kwenye matamasha mbalimbali kama unavyoweza kuona hapa…. https://youtu.be/G2ZKsHYc5yU na unaweza kuona live concert kwenye tamashala live la Jazz Tokyo hapa…. https://youtu.be/tZEPJ42hvNM

5.Ni vikwazo na changamoto gani ulikumbana navyo huko Japan wakati ukianza kazi yako huko Japan?

Lister anajibu;Changamoto ni nyingi na zote zilihusiana na maisha ya ugenini kama vile;

(a).Lugha-Mwanzo ilikuwa vigumu kwani wa-Japani hawaongei Kiingereza mpaka nilipoijua lugha yao changamoto nyingi zikaanza kupungua.

(b).Maandishi yao yako based on characters na si alphabet hivyo kujifunza hizo characters za kanji,katakana na hiragana zimenichukua miaka mingi ya kujifunza.

(c)Ubaguzi wa rangi bado upo-upo Duniani na Japan haina tofauti na nchi nyingine japo,miaka ya karibuni kwenye miji mikubwa ubaguzi unaelekea kutoweka ama kupungua taratibu.


                                                                 Akiwajibika jukwaani.

6.Je unaonaje maendeleo ya muziki wa dansi nchini Tanzania?

Lister anajibu;Maendeleo ya muziki wa dansi Tanzania naona ni ya kusua-sua kwani ile enzi ya wanamuziki ‘’kukuna vichwa kwa ubunifu’’imetoweka,kuiga muziki wa chi jirani kumeshamiri,bendi karibu zote zinapiga muziki unaofanana na si rahisi kupambanua bendi hii na ile ,kukosekana kwa ubunifu kumefanya hata wapiga vyombo kuiga style ya Wenge Musica na hivyo kuwa na miziki isiyo na rangi tofauti na bendi nyingine.

7.Ni bendi ipi na mwanamuziki yupi anayekuvutia Tanzania?.

Lister anajibu;Binafsi napenda kuangalia na kujifunza kutoka kwa’’ wanamuziki wa kimataifa’’ kuliko kuangalia wanamuziki wa nyumbani kwani nilitoka kitambo kwenye ‘’daraja la kitaifa’’ kwani kwa kiwango cha muziki wa nyumbani Tanzania,kama yapo ya kujifunza ni machache,hivyo nguvu zangu nimezielekeza kwenye ‘’ jukwaa la kimataifa’’ na wanamuziki wa kimataifa’’. 
                                                                Akivicharaza vinanda.
 
 8.Baadhi ya wanamuziki wa dansi nchini Tanzania nidhamu yao inaonekana kushuka siku hadi siku,unalionaje suala hili?

Lister anajibu;Nilikuwa nyumbani kipindi fulani mwaka jana / juzi,nilizunguka kuziona bendi karibu zote kubwa,niliona utovu mwingi wa nidhamu jukwaani,mfano baadhi ya wanamuziki kuchelewa kuingia jukwaani,kuitaita majina ya wateja katika hali ya kuwapandisha mori ama kuwahamasisha wateja hao watoe kitu,kuvuta sigara,kuongea na simu wakati mazoezi yakiendelea na mengine mengi yafananayo na hayo ambayo hayafai kwa kazi yetu ya muziki hususan wa dansi.

9.Unatarajia kurudi lini nyumbani kufanya shughuli zako za muziki ukiwa katika ardhi ya nyumbani?

Lister anajibu;Sina matarajio ya kurejea nyumbani hivi karibuni,kwani hakuna uhaba wa kazi nilipo,kama kurudi, nitarudi panapo majaliwa ya mwenyezi Mungu lakini si kesho wala keshokutwa.

10.Unadhani kuna sehemu ambayo unaona serikali inaweza kusaidia kuinua muziki?kama ipo ni ipi?

Lister anajibu;Kwenye mahojiano yangu mengi na vyombo vya habari TZ,nimependekeza mara nyingi kuwa serikali inatakiwa kuanzisha masomo ya muziki kwenye mitaala ya shule za msingi,elimu ya muziki haipo Tanzania na hivyo kupelekea matumizi ya vipaji pekee.

*Vipaji vikipaliliwa na elimu matokeo yatakuwa bora zaidi,vipaji pekee vinakuwa na ukomo* hasa kama mwanamuziki anataka kuwa na kiwango cha ki-mataifa.

                           Hii ni katika live concert katika Jiji la Tokyo nchini Japan.


11.Unawashauri nini wanamuziki na wadau wa muziki nchini?

Lister anajibu;(a)Kwa wanamuziki ni kwamba tujenge tabia ama mazoea ya kujisomea vitabu vya muziki na kujiendeleza zaidi kitaaluma .

(b)Kwa wadau-Tujifunze kuzikosoa tabia zisizopendeza za *BAADHI* ya wanamuziki kama kuomba-omba mahali pa kazi pia kuzikosoa kazi zao pale tusipofurahishwa,itakuwa changamoto nzuri na hao wanamuziki BAADHI watashituka na kuchukua hatua kujirekebisha kitabia na kikazi.Hapa nasisitiza "SI WANAMUZIKI WOTE WENYE KASORO HIZO".

12.Kaka Lister Elia tunakushukuru sana kwa muda wako,tunakushukuru sana kwa maelekezo yako kwa serikali,wadau na wanamuziki,karibu sana na usisite kutoa ushirikiano pale tutakapokuja kukuomba taarifa yoyote inayohusu muziki na maisha.

Lister ;Shukrani kwa kunikaribisha kwa pamoja tutalisukuma gurudumu la kavasha lisonge mbele.
                                      

                         KAVASHA GROUP YAKUTAKIA MAISHA MEMA NA KAZI NJEMA.





0 comments:

Post a Comment