LATEST POSTS

Saturday, August 15, 2015

MJUE OTHMAN MAJUTO,MWANAMUZIKI MPIGA BESI MTOTO WA KING MAJUTO .







                                                      

                                                     NDG OTHMAN KING MAJUTO.

Kwa mara nyingine kona yako ya Kavasha imekutana na nyota mwingine katika tasnia hii ya muziki wa dansi nchini na hapa imekutana na Ustaadh  Mwanajeshi wa  zamani  Othman Majuto mpiga gitaa la besi hodari nchini,Kwa kuongeza nguli huyu ni mtoto wa Msanii maarufu wa Maigizo na Vichekesho nchini Tanzania hapa namuongelea  Amri Athumani maarufu kama King majuto,Kama ilivyo ada hatukumuacha  hivi hivi Kavasha ilimbamiza maswali kadhaa na yeye bila hiyana alitupatia majibu yake,twende sasa;


KAVASHA; Habari yako kaka Othmani,Tungependa utupatie Historia yako kwa ufupi?

OTHMAN; Mimi ni mtoto wa kwanza wa Mzee Majuto,nilizaliwa mjini Tanga eneo la Makorora na kupata Elimu mkoani Tanga pia.



                 MZEE AMRI ATHUMAN''KING MAJUTO'' BABA WA OTHMAN

 KAVASHA; Lini ulianza muziki na ni Bendi gani ulizopitia?

OTHMAN; Nilianza muziki mwaka 2000 na walimu wangu ni Miraji Shakashia na Afande Mohamedi Mgollo,Bendi nilizopitia ni pamoja na Mwenge Jazz wana Paselepa,Mchinga Sound wana Timbatimba,Kalunde Bendi na Twanga Chipolopolo,Pia nimeshafanya namakundi mendi ya Muziki wa dansi asilia kama Mjomba Bendi ya Mpoto na 2mbili Bendi ya Zanzibar.


    MIRAJI SHAKASHIA WA THE AFRICAN STARS AMBAYE NI MWALIMU WA                                           GITAA WA OTHMAN MAJUTO

KAVASHA; Nini tofauti ya muziki wa dansi wenye vionjo vya asili na muziki wa dansi la kawaida tulilozoea?

OTHMAN; Kuna tofauti kubwa kwa kuwa muziki wenye mahadhi ya asili unabeba pia utamaduni wetu na kuwa kitambulisho kwa wageni,mfano Bendi ya Tatunane ama Wanne Star,vilevile  Inafrika Bendi na Kilimanjaro Bendi utaona kuwa tunapoteza muda na kuuzika utamaduni wetu kwa kuendekeza muziki ambao haubebi utamaduni wetu,yapasa tubadilike.
                    
                


             


                             OTHMAN MAJUTO AKIWAJIBIKA JUKWAANI.


KAVASHA; Mzee wako Mzee King Majuto ni Alwatan katika sanaa ya vichekesho,imekuaje ukajikita katika Muziki wa Dansi?

OTHMAN; Baba alikua akiimba katika maigizo yake kwa hisia mpaka watu wanalia ukumbini enzi hizo,hata hivyo nina vipaji vingi lakini hiki cha kupiga gitaa inaonekana kumeza vingine,ninacheza filamu katika kundi la Sisi na Tanzania na kazi iliingia sokoni nilicheza kama mesenja,ninachekesha pia.



KAVASHA; Muziki wa dansi nchini unakua ama unauonaje?

OTHMAN; Umedumaa,hadi hapa tulipo tushukuru juhudi za wanamuzikiwetu wa zamani kwa kazi nzuri walioifanya ammbayo yatupasa kuitendea haki kwa kufanya kazi kwa bidii na heshima ili kusogeza hatua mbele toka pale walipoishia hususani kujikita katika midundo asilia kwani tuna hazina kubwa ya makabila yenye nyimbo na midundo mizuri inayofaa kutumika kutoa burudani ili mradi tu ifanyiwe marekebisho kidogo na kutumia ala za kisasa.


               

                                       OTHMAN MAJUTO AKIWAJIBIKA.

KAVASHA; Ni Nchi gani ambazo uliwahi kutembelea kwa kwenda kufanya kazi yako ya muziki na nini yalikua mapokeo kwa kazi yenu huko ughaibuni?

OTHMAN; Nchi nilizowahi kutembelea kikazi ni nyingi lakini kwa uchache ni kama vileMiji ya Mombasa na Nairobi nchini Kenya,Kampala Uganda,Maputo Mozambique,Dubai UAE,Muscat Oman na Mumbai India,kote huko kazi yetu ilipokelewa kwa mikono miwili.


                 
               
                                                  OTHMAN KING

KAVASHA; Familia ya muigizaji mkubwa nchini Je kuna mwingine ambaye ni msanii ukiondoa wewe na Mzee Majuto?

OTHMAN; Ndio wapo wadogo zangu kina Muddy King,Haruna King,Hamza King,Bilali King na Abuu King Majuto ambao wote hao ni wacheza filamu.


KAVASHA; Nini Manufaa uliyoyapata kutokana na kazi ya muziki?

OTHMANI; Manufaa yapo kama vile kujipatia rizki halali ya kila siku,kujipatia ardhi kwa ajili ya makazi na pia mtaji kwa ajili ya biashara japo si kubwa kivile namshukuru mungu kwani muomba mola hachoki.


KAVASHA; Unaonaje Heshima ya wanamuziki hapa nchini imeshuka ama ipo juu,kwa nini?

OTHMAN;Heshima ya wanamuziki inashuka na bado itaendelea kushuka kama hatua za makusudi hazitachukuliwa na wanamuziki wenyewe.
Sababu kubwa ya kushuka kwa heshima ya wanamuziki ni-

1.Kukosa maadili kwa kucheza nusu uchi majukwaani mbele ya kadamnasi jambo linaloleta tafsiri tofauti mwishowe ni dharau.

2.Hatuna umoja,majungu na fitina ndio zimetawala katika jamii yetu.

3.Media nazo zinachangia kwa kiasi fulani kushusha muziki wa dansi,Bila Rushwa nyimbo yako ya dansi haipati muda wa kupigwa(airtime)badala yake wamejikita katika Bongofleva  ambapo wanamuziki wake kwa asilimia kubwa hawaujui vema muziki na ama kwa hakika muziki bora na wenye weledi na kuburudisha ni wa LIVE BAND ambao katu huwezi fananisha na  Bongo fleva asilani abadani.

              
                             
                                                LIVE BAND


KAVASHA; Ukiambiwa taja mwanamuziki mmoja na Bendi moja ambaye na ambayo ni bora kwako wewe ungesemaje?

OTHMAN; Kwangu mimi Bendi bora ni The Kilimanjaro Wana Njenje na Mwanamuziki Bora kwangu ni Wazir Ally pia kutoka Njenje.


    WAZIR ALLY WA KWANZA KULIA AKIWA NA THE KILIMANJARO BENDI WANA                                                     NJENJE

KAVASHA; Ni nini Ushauri wako kwa wanamuziki na wamiliki wa bendi nchini Tanzania?

OTHMAN; Nawashauri wanamuziki wenzangu tupendane na tuongeze juhudi katika kazi ili kuongeza thamani yetu.
Nawashauri wamiliki wa bendi nchini wathamini jasho la wanamuziki wao,kujali utu na kipato chao ili kuongeza tija kwa maendeleo ya pande zote mbili,lakini pia tuthubutu kwa dhati kutumia makabila yetu kuweka vionjo vya asili katika midundo yetu jambo ambalo litatambulisha kazi zetu nje ya nchi na kuziuza huko na kupatia Nchi yetu pato pamoja na wamiliki wenyewe na  wanamuziki pia,mfano nchi za Afrika magharibi muzikiwao hujulikana kiurahisi na kuwa kitambulisho kwa utamaduni wa nchi zao.


Ndugu Othman Majuto tunashukuru sana kwa ushirikiano wako na tunakukaribisha tena katika jukwaa letu la KAVASHA GROUP TANZANIA.

       OTHMAN KING MAJUTO ANAPATIKANA KWA MAWASILIANO HAYA
                                   
                                SIMU NO  +255 658 967 366
                   
                                     



0 comments:

Post a Comment