MGENI WETU HII LEO NI FAIDA ONGALA WA AKUDO IMPACT
Faida Remmy Ongala.
Blog pendwa ya Kavasha leo imepata bahati ya kukutana na
mwanamuziki anaekuja kwa kasi ambae pia ni binti wa mwanamuziki mkongwe wa
miondoko ya dansi Marehemu Dokta Remmy Ongala,huyu si mwingine bali ni Faida
Ongala,Kavasha Blog ilikua na machache iliyohitaji kujua toka kwake kwa ajili
ya wasomaji wa wake na mazungumzo yalikua kama ifuatavyo;
1.Kavasha Blog; Dada
Faida wasomaji wa blog hii pote duniani wangependa kujua mawili matatu toka
kwako,wewe ni nani na historia yako ya muziki mpaka sasa,bila shaka upo tayari
kutujuza,karibu sana.
Faida; Asante sana
nipo tayari kuwajuza,Mimi naitwa Faida Remmy Ongala,ni miongoni mwa watoto wa
Marehemu mwanamuziki Dokta Remmy Ongala,nilipenda muziki toka zamani nikiwa
mdogo,nilivyomaliza masomo ya Sekondari nilijiunga na chuo cha muziki kiitwacho
Evelyne Music School kilichopo Kimara bucha baada ya kusoma miezi mitatu
nikahamia chuo cha DHW Country Music
Academy kilichopo Zanzibar baada ya kuona kuna unafuu wa ada,Nashukuru
Mungu baada ya kuwa nafanya vema katika masomo nikapata wafadhili ambao walinisomesha
bure kipindi chote ambachonilikua nikisoma hapo,nilisomea kupiga gitaa na ngoma za asili na kucheza
pia na baada ya Chuo hicho cha Zanzibar nilikwenda Ethiopia ambapo nilisoma kwa
miezi minane ambapo mpaka sasa nimemaliza masomo kwa jumla ya miaka mitatu ya
masomo mbalimbali ya muziki kama nilivyoyataja katika vyuo vyote vitatu toka Dar,Zanzibar hadi Ethiopia.
Faida Ongala akifanya mazoezi nyumbani kwake.
2.Kavasha Blog; oohh
historia nzuri kabisa bila shaka ni mwanamuziki msomi Faida
Faida;anacheka….asante ni msomi kiasi ,yafaa sisi wanamuziki
tupate elimu kidogo juu ya muziki ili kujua kwa undani muziki ukijumlisha na
vipaji vyetu.
3.Kavasha Blog; Ni
nini ulichokipata kutoka kwa baba yako marehemu Dk Remmy Ongala kuhusiana na
muziki?
Faida anajibu;Nimejifunza na kupata vitu vingi toka kwa baba
angu mzee Remmy kama vile kufanya juhudi katika kazi yangu ya muziki kitu ambacho nakifanya ili kuweza kufikia
mafanikio yake yeye ama mara mbili zaidi ya pale alipofikia,kitu kingine
alipenda kazi yake na mie pia ninaipenda kazi yangu katika mazingira na namna
zote zile na kingine nimerithi kipaji chake cha muziki na kuwa mwanawe wa kike
wa pekee niliye katika fani hii ya muziki.
Baba wa Faida,Dr Remmy Ongala.
4. Kavasha Blog; Ni
muziki gani unaumudu ?
Faida;Namudu miziki mingi na sipigagi miziki michache kama
singeli,hiphop,taarab,michiriku nk.
5. Kavasha Blog; Baba
yako Dk Remmy alitumia kauli kali kutetea alichokiamini mfano wimbo muziki asili yake wapi kuna
maneno haya’’muziki sio uhuni,kama muziki ni uhuni kwa nini unanunua
kaseti,unacheza muziki ama unaomba nyimbo redioni,je unawaambia nini wanaodhani
muziki ni uhuni?
Faida; Ni kweli muziki sio uhuni,muziki ni kazi kama kazi
nyingine na inapaswa kuheshimiwa na watu wasifikiri kuwa kila afanyae muziki ni
muhuni la hasha,uhuni ni asili ya mtu ndio maana watu wanaofanya kazi katika
ofisi zenye heshima utakuta ni wahuni,vizazi vya washika dini navyo utakuta
kuna wahuni waliobobea na hata watoto wa matajiri wasio na shida ya chochote
utakuta ni wahuni kupita wanamuziki hivyo napenda wadau wa muziki na wale walio nje ya muziki wafahamu kuwa
muziki sio uhuni ni kazi nzuri na ya ujuzi mkubwa kama ama zaidi ya kazi ya
baadhi ya wanobeza kazi ya muziki.
Faida Ongala akijiandaa kupanda jukwaani Nchini Dubai.
6. Kavasha Blog; Vipi
kuhusu familia umeolewa?
Faida;Mimi sijaolewa na sina mtoto,ninaishi na familia yangu
inayojumuisha mama na ndugu zangu wengine.
7. Kavasha Blog; Uliwahi
kufanya kazi na bendi ama makundi gani na sasa upo na kundi gani?
Faida; Niliwahi kufanya kazi na kundi la kaka zangu Godfrey
na Thomas katika Band yao inayojulikana kama Ongalas Band ,nikatoka kwa kaka
zangu ili kujitafutia changu mwenyewe maana kutegemea cha ndugu sana ni tatizo na
pia kuongeza uzoefu ambapo nilikwenda Dubai kujiunga na Band iitwayo 2extra
Ngwasuma ambapo nimerudi na kujiunga na Band ya Akudo Impact vijana wa
masauti,pia ninaweza kupiga kama solo artist,nimepita pia kundi la ndege watatu
kwa muda mfupi.
Hili ni kasha la wimbo wake wa UMEBADILIKA.
8. Kavasha Blog; Unaonaje
maendeleo ya muziki hususani wa dansi nchini?
Faida; Kusema kweli muziki kwa hapa Tanzania umeshuka
kiwango hasa muziki wa dansi,unajua muziki wa
dansi unategemewa na wanamuziki wengi na hata wasio wanamuziki kwa
sababu unatoa ajira kwa watu wengi kwa wakati mmoja kuliko aina nyinginezo za
muziki kama vile Bongofleva nk, hivyo muziki wa dansi unavyoendlea kushuka inakua mbaya
sana kwa wanamuziki na wadau kwea namna moja ama nyingine.
9. Kavasha Blog; Tangu
kifo cha Mzee wako Dokta Remmy ile staili yake ya kutoa usia na kukemea maovu
katika jamii na kupongeza wale waliofanya mazuri na wenye uthubutu hakika
imepotea,ukiwa wa damu yake una mpango wa kufata nyayo zake?
Faida;Ndio nina mpango huo kwa sababu nilikua napenda
alivyokua anawaambia ukweli watu na viongozi wazembe,mfano wimbo niseme nini
ambao anasema ‘’saa mbili asubuhi,foleni kwenye supu,ofisi ipo na nani bwana
weee’’ukiangalia wanamuzki wengi hasa wa kizazi kipya(bongofleva)wamejikita
zaidi kwenye nyimbo za mapenzi lakini mimi nitafata nyayo za baba ili niweze
kuelimisha wananchi katika jamii na walimwengu kwa ujumla kama alivyofanya
baba.
Marehemu Dokta Remmy Ongala wakati wa uhai wake.
10. Kavasha Blog; Nini
malengo yako ya baadae?
Faida anajibu; Natarajia kuwa mwanamuziki mkubwa sana
kitaifa na kimataifa,pia niweze kufikia malengo yangu ninayoyawazia na kufanya
vizuri katika tasnia hii ya muziki.
Faida Ongala akipozi wakati wa mapumziko.
11. Kavasha Blog; Unawaambia
nini wadau,Serikali na wanamuziki kwa ujumla kuhusu kuinua muziki wa dansi na
mingine kwa ujumla?
Faida anajibu;Jamani muziki wa dansi ni muziki wa toka enzi
na enzi,umetumika sana katika shughuli za kitaifa na kimataifa kama wimbo
Zimbabwe wa DDC Mlimani Park ukizungumzia uhuru wa Zimbabwe,naiomba
serikali wajaribu kukaa na wadau wa muziki na wanamuziki kuangalia nini cha
kufanya ili kurudisha hadhi ya muziki wa dansi nchini,pia nawaasa wanamuzki
wote kuwa kitu kimoja bila kujali tofauti za makundi yao,ushrikiano ni jambo la
msingi katika maendeleo yetu na pia kuupandisha muziki huu wa dansi.
Kavasha Blog; Tunakushukuru
Lady Doctor Faida Ongala kwa ushirikiano wako natumai tutaendelea kuwa pamoja
siku zote.
Faida ;Asante na mie nafurahi kuzungumza na Blog ya kundi la
Kavasha Group Tanzania.
KILA LA HERI
DADA FAIDA ONGALA
ANAPATIKANA KWA SIMU NAMBA ZIFUATAZO
ANAPATIKANA KWA SIMU NAMBA ZIFUATAZO
+255715023646 KIKAZI ZAIDI.
0 comments:
Post a Comment