LATEST POSTS

Wednesday, July 15, 2015

ZAHIR ALLY ZORRO;TUMERUDI KISHUJAA ULIIMBWA KAMA WIMBO WA TAIFA.


Leo hii Kavasha Blog imekutana na nguli ama manju wa muziki wa dansi nchini,si mwingine bali ni 
Zahir Ally Zorro(pichani),kabla ya Kavasha Blog kumuuliza mawili matatu Mzee Zahir alipata fursa ya kutueleza yeye ni nani,na ametoka wapi na anaelekea wapi katika maisha yake ya kimuziki,Alisema;


‘’Naitwa Zahir Ally Zorro,nilizaliwa Dar-Es-Salaam mtaa wa Dr Kirck sasa ukijulikana kama mtaa wa Lindi,Gerezani,ni mtoto wa kwanza kwa Baba yangu Mzee Ally Ahmed Mulloh Sing Suleiman Zorro na Bi Pili Banana Muhammad.
 

Nilisoma Kindergatten ya TAPA, Mwaka 1959 nilisoma Midldle 1&2  na Mwaka 1960 nilipelekwa Tabora kusoma dini masomo ya Koran Tukufu,Mwaka 1962 nilianza masomo ya elimu ya msingi katika shule ya Msingi Kaze Hill Uper Primary School karibu na shule ya Sekondari ya Wasichana na si mbali sana na Tabora Boys Sekondari sikusoma la pili nikarushwa la Tatu kutokana na ufahamu.


Mwaka 1964 ilikua nadhani Mwezi wa Aprili nikarudishwa Dar- Es-Salaam Shule ya Mtaa wa Kisarawe eneo la Gerezani ambapo nilimaliza mwaka 1968. Baada ya hapi ndipo safari yangu ya muziki ilipoanza ambapo nilikwenda Mwanza na kujiunga na Bendi ya Super Vea kuanzia Mwaka 1969 hadi Mwaka 1973.Na baada ya muda mfupi nilijiunga na Mara Jazz ambapo sikudumu sana kwani  niliamua kurudi  nyumbani kwa Mama yangu Mtaa wa Muhonda no 22 Dar Es Salaam.
 

Mnamo Mwezi Novemba 1,1973 niliajiriwa Jeshi la Kujenga Taifa ambapo nikiwa Mwanajeshi kamili nilishiki katika Bendi ya Jeshi hilo iliyojulikana kama KIMULIMULI Orchestra,nilidumu Jeshini hadi Mwaka 1989 nilipoamua kuacha kazi na moja kwa moja nikaenda kujiunga na Bendi ya Sambulumaa niliyodumu nayo kwa muda mfupi kwani Mwaka 1990 nilijiunga na Bendi ya Washirika Tanzania Stars niliyodumu nayo hadi Mwaka 1995 Bendi hiyo ilipovunjwa nikawa Mwanamuziki wa kujitegemea,pia nimewahi kuanzisha Bendi yangu ya Mass Media ambayo ilivuma kwa wimbo wake wa Beatrice Affairs,Pia nilipata kumsapoti Banana Zorro ambaye ni mwanangu pale alipoanzisha Bendi katikati ya Miaka ya 2000,Nimepigapiga Hotelini pia.
Kwa sasa nimenunua vyombo vyenye thamani ya shilingi milioni 40 na hivi nguvu ya kifedha imepungua nasubiri wafadhili walioniahidi Tshs M5 ili nianzishe tena Bendi yangu ya Mass Media Extra Ball’’.


Mzee Zahir Ally Zorro akiwa na wadau wa Muziki wa Dansi kutoka kushoto ni John Shekwavi,MzeeJuma Kihenge na Mbarouk Nyambi.


Naam historia fupi kabisa lakini ni nzuri sana,muda umewadia kukukuliza  maswali machache ili kuwajuza Wanakavasha na wapenzi wote wa muziki Duniani Kavasha Blog inapowafikia.


1.KAVASHA-SWALI:Unazungumziaje muziki wa dansi hivi sasa umepanda au umeshuka kulinganisha na na miaka ya nyuma?

ZAHIR ZORRO-JIBU;Muziki wa Dansi ni kama haupo.


2.KAVASHA-SWALI:Ni nichi zipi ambazo uliwahi kufanya kazi yako ya muziki ?

ZAHIR ZORRO-JIBU;Nimefanya kazi katika nchi za Kenya,Dubai,Uganda,Zambia,Afrika ya Kusini,Iran na nimetembelea nchi nyingi za Kiarabu.

3.KAVASHA-SWALI:Wimbo wa Tumerudi kishujaa unaakisi vita ya Uganda na Tanzania,ni upi ushiriki wako katika Vita hiyo?

ZAHIR ZORRO-JIBU;Wimbo huo niliutunga na kuimba lead vocal baada ya kwisha kwa vita ya kumng’oa Nduli Idd Amin.


4.KAVASHA-SWALI:Katika tungo zako zote kama Cleopatra,Photo Album,Kisura,Beatrice Affairs nk ni ipi ambayo ukiisikia mwenyewe inakusisimua na kwanini?

ZAHIR ZORRO-JIBU;Ni TUMERUDI KISHUJAA,kwa sababuni ni  wimbo wenye hadhi ya juu na wenye hadhi ya wimbo wa Taifa maana hata leo ukiimbwa utasikia kitu kinagonga moyoni.


5.KAVASHA-SWALI:Ni mtindo gani unatarajia kutoka nao katika Mass Media Extra Ball ujio mpya?
ZAHI ZORRO-jibu;Bado sijaamua maana litasubiri nione niaina gani ya kikosi nilichonacho.


6.KAVASHA-SWALI:Unazungumziaje tatizo la maslahi kwa wanamuziki na nini suluhu ya tatizo hilo?

ZAHIR ZORRO-JIBU;Tatizo ni kutokua na umoja baina ya wanamuziki na suluhu ni kufanya kazi kwa bidii,kazi ikiwa bora wamiliki watakutafuta na utapanga maslahi yako,kazi ikiwa mbaya utatafuta ajira na utapangiwa maslahi,pia mshikamano ni muhimu kwa wanamuziki.


7.KAVASHA-SWALI:Ukiondoa watoto wako Banana na Maunda,je kuna mwingine aliefata nyayo zako?

ZAHIR-JIBU;Nina watoto 10 lakini waliofata nyayo ni hao wawili tu.




8.KAVASHA-SWALI:Kipi kinakufanya uonekane na uonekano huohuo kwa muda mrefu kama kijana Zorro?

ZAHIR ZORRO-JIBU,Kwanza ni kudra za mwenyezi mungu,lakini pia ni hali ya mzoezi niliyopata kupitia nikiwa jeshini pengine,namshukuru Mungu kwa yote.


9.KAVASHA-SWALI:Nchini Kenya uliwahi kufanya kazi na Bendi zipi?

ZAHIR ZORRO-JIBU;Kenya nilirekodikwa lebo ya Le  Grand Kizza iliokua na mtindo wa Kizaizai,pia nilikuja kusaidia kuanzisha Bendi ya Simba Wanyika maana ilikua imekufa,hivyo nilikua pia mwanamuziki wa Simba Wanyika.


10.KAVASHA-SWALI:Umefanya kazi na wanamuziki wengi,tutajie kwa uchache uliopata kufanya nao kazi?

ZAHIR ZORRO-JIBU;SAMBULUMAA- nilifanya kazi na Nguza Vickings,Mulumba Tomaa,Bakari Mlanzi,Lollo Leonard toka OK Jazz,Bikassy Mandeko toka Kinshasa,Kasaloo na Kyanga songa,Mohamedi Gotagota,Joseph Maina,Skassy Kasambula nk.
KIMULIMULI-Niliimba na Zacharia Fanuel Mabula aliyetokea Western Jazz alieimba wimbo wa vigelegele na nyinginezo za Western Jazz na wengineo.
WASHIRIKA STARS-Nilifanya kazi na kina ALLY Choky,Mwinjuma  Muumin,Musemba wa Minyigu,Mohamedi Shaweji nk
SUPER VEA- Nimefanya kazi na Mussama Andre ambaye ndie hasa mwalimu wangu wa muziki.
SENSERA-Juma Nguzo na Juma Habibu na wengine weeeengi sana ambao humu hawatoshi.

MUUMIN MWINJUMA NA ALLY CHOKY WALIPATA KUFANYA KAZI NA MZEE ZORRO



11.KAVASHA-SWALI:Ni zipi nasaha zako kwa Wanamuziki wa muziki wa Dansi nchini?

ZAHIR ZORRO-JIBU;Muziki huu unaweza kusimama iwapo wanamuziki watajituma zaidi na zaidi,nidhamu kazini na kufanya workshop ambayo kwayo itasaidia kubadilishana ujuzi,kuanguka kwa wakongwe wa muziki nako ni tatizo lakini waliokuwepo wanaweza kwa namna moja ama nyingine wakikumbukwa kwa ushauri na kadhalika wanaweza kusaidia kuinua tena muziki wa dansi.


12.KAVASHA-SWALI:Nini wito wako kwa Serikali?

ZAHIR ZORRO-JIBU;Serikali  imesahau kidogo muzikiwa dansi,tunaiomba iusaidie muziki huu ili uweze kurejea makali yake ya zamani na pia iyaruhusu mashirika yake yarudishe kitengo cha burudani kama ilivyokua Shirika la Bima na Kiwanda cha nguo cha Urafiki na mashirika mengine mengi,ingawa naona kuna matumaini kwa huyu alieteuliwa na CCM Ndugu John P.Magufuli kama atapita anaweza kukumbuka tasnia hii ya muziki wa Dansi kwani ameonesha mahaba yake kwa muziki waziwazi.




MH JOHN MAGUFULI AKIPIGA TUMBA NA WANAMUZIKI WA MSONDO

KAVASHA BLOG TANZANIA-Tunakushukuru kwa kutoa muda wako na kuujuza umma mambo tofautitofauti,ahsante na karibu tena.

ZAHIR ZORRO-Asanteni sana nawatakieni shughuli jema,mbarikiwe.
       

  MZEE ZAHIR ALLY ZORRO ANAPATIKANA KWA MAWASILIANO YAFUATAYO.
                                              SIMU NO:0713-661717
                                  EMAIL ADRESS-zahirallyzorro@gmail.com







4 comments:

  1. Shukran kwa historian hiyo. Nimejifunza mengi kupitia hiyo makala

    ReplyDelete
  2. Thanks for giving us that story,its very nice and reminds us alot of the years back.

    ReplyDelete