LATEST POSTS

Saturday, July 18, 2015

HATIMAYE BANZA STONE AZIKWA,R.I.P BANZA.

http://www.johnkitime.co.tz/wp-content/uploads/2015/06/Banza-Stone.jpg

                                   
                                                Ramadhani Masanja ''Banza Stone''

Hatimaye nyota wa muziki wa dansi  nchini Tanzania Ramadhani Masanja''Banza Stone''aliyefariki Dunia hapo Jana nyumbani kwao Sinza Kijiweni baada ya kuugua kwa muda mrefu,amezikwa leo katika mazishi yaliyohudhuriwa na umati mkubwa wa watu wakiwemo wanamuziki wenzake,wanasiasa,wasanii wa filamu na watu kutoka Taasisi binafsi na za Serikali na mashabiki lukuki.

Hali ya simanzi ilitanda katika mazishi hayo ambapo nyuso za wengi zilionekana kugubikwa na huzuni kubwa.

Banza alianza kuingia katika masuala ya muziki kama dansa wa kundi la Home Boys mwanzoni mwa miaka ya tisini kisha kupitia katika Bendi ndogondogo za Afriswezi na Twiga njia iliyomfikisha Bendi ya African Stars wana Twanga Pepeta ambapo alitamba kwa Tungo kadhaa ikiwemo Kumekucha na Aungurumapo Simba kabla ya kuchukuliwa kwenye kundi la CCM la TOT kwenda kuimarisha masuala ya Propaganda ambapo aliinua vema kwa vibao moto kama Mtaji wa Masikini,Jahazi,Tushirikiane na Baadae Aungurumapo Simba Remix na Elimu Ya Mjinga.

Pia aliwahi kuongoza Bendi yake binafsi katika vipindi viwili tofauti iliyojulikana kama Bambino Sound akitamba na vibao kama Maneno maneno na Mimi niseme na wewe useme,Pia alipita katika Bendi ya Extra Bongo alipoachia kibao cha Falsafa ya mapenzi na Bendi yake ya mwisho ambayo haikudumu kwa muda mrefu ilikua Rungwe Bendi.

     
     Uelekeo kwenda katika makaburi ya Sinza kwa mazishi.


Atakumbukwa kwa kazi binafsi za Zingzong kama ile ya mafahali watatu aliyofanya na wenzake kipindi hicho waliokua katika chati ya juu mno Ally Chocky na Mwinjuma Muumin ambapo alitoa wimbo wa Mungu ni wetu sote,Pia akatoa katika zingzong na Ally Choky katika sisi ndio sisi na kutoka na Winnie pamoja na Mshenga,anakubukwa pia kwa kazi binafsi aliyomshirikisha Malou Stonch KUMEKUCHA REMIX yenye vibao kama Kumekucha,Nilipoanza,Familia,Toka Mpenzi,Leoleo, na Sintokubali.


Amepata kufanya kazi binafsi pia na Marehemu Suleiman Mbwembwe na Adolf Mbinga katika Neema  Remix ambayo ilipigwa awali na Bendi ya Diamond Sound na nyingine nyingi tu binafsi na kushirikishwa.


Banza alizaliwa tarehe 20 Oktoba 1972 mwezi wa Ramadhani na kufariki jana Tarehe 17 Julai 2015 siku ya mwisho ya Ramadhani na kuzikwa siku ya Eid El Fitr hakika hii ni Rehema kubwa,tumuombee mwanazuoni huyu kauli thabiti inshallah.

     Wakati mgumu wa Kuzikwa kwa mpendwa wetu Banza
       
 TUNASEMA KWA MUNGU TUMETOKA NA KWAKE YEYE TUTAREJEA

    R.I.P JENERALI BANZA STONE

0 comments:

Post a Comment