LATEST POSTS

Tuesday, December 1, 2015

SAFARI YA KIMUZIKI YA ABETHY MASIKINI.

 
BY DAUDI KISUGURU


SAFARI YAKE YA KIMUZIKI NA HARAKATI ZAKE
MWANAMUZIKI MWANAMAMA

ELISABETH FINAT AL MAARUFU
KAMA ABETI MASIKINI

ABETI MASIKINI ni mwanamuziki aliyefanya kazi kubwa ya kuwaibua baadhi ya wanamuziki waotamba hivi sasa huko jamhuri ya kidemokrasi ya congo (DRC) jina lake kamili ni ELISABETH FINAT alizaliwa Novemba 9,1954 katika mji wa KISANGANI mashariki ya congo (DRC).
Abeti alitokea katika familia ya watoto wanane,Baba yake JEAN FINAT alikuwa chotara wa kibelgiji.
Mwaka 1961,Abeti alipata pigo baada ya baba yake kuuawa kikatiri mjini MBUJIMAYI kutokana na matatizo ya kisiasa.Finat alikuwa mwanachama wa chama cha MLC,
kilichokuwa kinaongozwa na PATRICE EMERY LUMUMBA,
aliyekuwa waziri mkuu wa zamani wa DRC LUMUMBA ndiye shujaa wa uhuru wa nchi hiyo.Hali hiyo ilimfanya mama yake Abeti kuchukua uamuzi wa kuhamia katika jiji la KINSHASA ili apate kujihifadhi akiwa na wanawe.


Walipofika kinshasa mama yake alimchukua Abeti na kumrejesha darasani katika shule iliyokuwa inajulikana kama "LYCEE YCEE SACRECEUR" kwa sasa inaitwa BOSONGANI,baada ya kumaliza shule ya sekondari akaajiriwa kama katibu kwenye ofisi ya waziri wa utamaduni.

Aliwashangaza baadhi ya ndugu zake na familia baada ya Abeti kuamua kuacha kazi aliyokuwa nayo na kuelekeza mawazo yake kwenye fani ya muziki na ndipo alipojipachika jina la betty.
Mwaka 1971 chini ya usimamizi wa mwanamuziki GERALD MADIATA, palitokea mashindano ya kumtafuta mwanamuziki chipukizi betty akaamua kushiriki kwenye mashindano hayo ambayo kwa bahati mbaya hakufaulu.


Hamasa ya kuupenda muziki ndipo ilipoongezeka huku akiwa mdogo akichipukia akiwa na umri wa miaka 17 tu, wakati huo ili apate kutumbukizwa katika unenguaji kwa jina hilo alilojipachika mwenyewe ilibidi ajiongezee miaka mitatu zaidi na kusema ana miaka 20.

ABET akisaidiwa na kaka yake JEAN ABUMBA ambaye alikuwa mpiga gitaa mashuhuri akawa kila siku anafanya maonyesho kwenye klabu ndogo ndogo jijini kinshasa abeti masikini alikutana na GERALD AKUESON aliyekuwa raia wa TOGO jijini kinshasa mwaka 1971 hapo ndipo fani yake ya ilipoanza rasmi.


GERALD AKUESON akawa ndiye meneja wake mkuu tangu mwaka 1972 Abet na Akueson wakaanzisha pia mahusiano ya kimapenzi na kufunga ndoa mwaka 1989 walifungia ndoa jijini PARIS UFARANSA na wakabahatika kupata watoto wanne wakike watatu na wa kiume mmoja, mumewe huyu alimshauri waongozane wahamie kwenye nchi za afrika magharibi ambako walitumaini kupata mafanikio zaidi
wakiwa huko walijikuta wana mashabiki wengi sana kwenye nchu za Benin, Cote d'ivore , Togo, Niger, Nigeria ,Guinea na Ghana.
Baada ya miaka kadhaa akiwa kwenye nchi hizo ,Abet masikini aliamua kurudi drc ambako hakupata mapokezi mazuri kwa kuwa watu wengi walikuwa hawamfahamu kabisa kilichomponza kwa kipindi hicho
chote alikuwa hajawahi kutoa albamu hata moja .Licha ya kutokufahamika kwake aliamua kufanya onyesho kubwa katikati ya jiji la kinshasa kwenye ukumbi wa CINE PALLDIUM ambako aliambulia watu 12 pekee ndiyo waliojitokeza kumuangalia.

Tukio hilo halikumkatisha tamaa aliendelea kufanyakazi kwa bidii ili malengo yakamilike ,baada ya kufanya mazoezi ya kutosha y kuboresha sauti yake mwaka 1973 alitoka na albamu yake ya kwanza ya "PIERRE CARDIN" ikiwa na nyimbo kadhaa ikiwemo ya "mutoto wangu" ,"bibile,"aziza","miwela" na "safariet papy yaka". albamu hiyo haikupokewa vizuri na wakazi wa kinshasa machoni mwao walimchukukulia kama mgeni na kumlaumu kwa tabia yake ya kuimba kwa kutumia lugha ya kiswahili.
Nguli huyu wa muziki abeti masikini akapata wazo la kuunda kundi lake akalipa jina la LES REDOUTABLE kundi hili lilikuwa na wanenguaji wake machachari waliojukana kama LES TEGRESS lililofanya watu wengi wavutiwe nae.

Maonyesho yake katika jiji la kinshasa yakawa gumzo mitaani kazi aliyokuwa anaifanya meneja wake ikaanza kuzaa matunda mema, alifanikiwa kupata mkataba uliomfanya kwenda kufanya onyesho katika ukumbi maarufu wa OLYMPIA ulioko paris, Nchini Ufaransa.


Mwaka 1973 akiwa njiani kuelekea kwenye onyesho hilo alitua katika jiji la DAKAR nchini SENEGAR huko alifanya onyesho lililohudhuriwa pia na rais wa nchi hiyo wa wakati huo RAIS LEOPOLD SEDAR SENGHOR pesa alizopata alizitoa kama msaada wake kwa watu walioathiriwa na ukame wa ardhi.

Alipotua Paris Februari 2,1973 aliporomosha bonge la shoo lililovutia watu hasa mashabiki wa kizungu kwenye ukumbi huo wa olympia Abeti masikini alifanikiwa kufanya onyesho lingine june 6,1974 kwenye ukumbi wa CARNEGIE ulioko katika jiji la NEW YORK nchini MAREKANI umaarufu wake ukazidi zaidi hususani pale alipopewa fursa ya kutumbuiza kwa pamoja na nguli wa muziki duniani katika jukwaa moja na mwanamuziki JAMES BROWN, 
MARIAMU MAKEBA ,TABU LEY na FRANCO LUAMBO MAKIADI kabla ya pambano la masumbwi la kihistoria kati ya MOHAMMED ALLY (Casius Clay) na GEORGE FOREMAN jijini KINSHASA.

Alifyatua albamu ya pili mwaka 1975 ikiwa na jina la "VOIX DU ZAIRE" nyimbo zilizokuwa zimesheheni ni "Likayabo","yamba yamba","bamba","nalikupenda","luliki" na "ngoyae" mwaka huo huo wa 1975 ndiyo Aliopokea mwaliko mwingine kwenda kutumbuiza katika ukumbi wa olimpia kutoka kwa COQUATRIX aliyekuwa mmiliki wa ukumbi huo ,akaenda kwa mara nyingine kufanya maonyesho mengine mawili kwa siku mbili mfululizo ndipo hapo alipopachikwa jina la Tiger mwenye kucha za dhahabu.
Mwaka 1976 ulikuwa mbaya kwake kimasilahi kwani alipata mpinzani wa uhakika katika muziki aliyejulikana kwa jina la MPONGO LOVE aliyekuwa juu kuliko yeye.


Mpogo Love akaongoza katika hili parade redio ya Taifa ya jamhuri ya kidemokrasia ya kongo (zaire) wakati huo,wimbo wake wa "pass possible" ulimfanya apendwe mno na mashabiki pamoja na yote mwaka 1977 Wanamuziki hao Abet masikini na Mpongo love walifanya kitu ambacho hakikutarajiwa na wengi pale walipofanya onyesho kubwa la pamoja kwenye ukumbi wa CINE PALLDIUM katika jiji la kinshasa na kuacha simulizi kubwa.Kwani kila mmoja akaimba kiaina yake wakaweka misingi mizuri ya kupendana kwa wanamuziki wa kike wa kizazi chao .


Historia ya Abet Masikini itaendelea kukumbukwa daima kwa yeye kuwa darasa tosha wanamuziki wengi maarufu wametokea kwake akiwemo Mbilia Bel aliyekuwa mnenguaji wake kuanzia mwaka 1976 mpaka mwaka 1981,loulina kanza aliyekuwa mpiga gitaa mwaka 1980 hadi mwaka 1981, Abby Surya aliyekuwa mnenguaji kuanzia mwaka 1984 mpaka 1986 , Malage de Lugendo aliyekuwa mwimbaji na wengine ni Joelle Esso, Tshala Muana nwaka 1978 mpaka 1979, Yondo Sister mwaka 1986 na Lambio Lambio"Komba Bellow".

Abet Masikini ni mmoja wa wanamuziki wa kike barani afrika waliofanikiwa kujiwekea jina kimataifa alidhihirisha uwezo wake wa kipaji chake na kufahamika nchini congo ambako muziki umetawaliwa na wanaume,Abet pia alikuwa mstari wa mbele kupigania haki za wanawake kwa mapenzi ya mungu ABET MASIKINI alifariki dunia septemba 9,1994 akiwa katika jiji la paris nchini Ufaransa 
tarehe hiyo inafanana na ile yake ya kuzaliwa novemba 9,1954.

MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALA PEMA PEPONI AMIN.

0 comments:

Post a Comment