LATEST POSTS

Sunday, July 5, 2015

JUAKALI WA TOT PLUS USO KWA USO NA KAVASHA


Juakali akiwajibika jukwaani

Leo kavasha imefanikiwa kukutana na mwanamuziki wa dansi anayeitwa Juakali ambaye tulifanikiwa kufanya naye mahojiano kuhusu historia yake na shughuli zake za muziki

SWALI 1.Ulizaliwa lini na wapi?

JIBU-Kwa jina naitwa Japhet Idriss Amir Mbaruku maarufu jina maarufu ni Juakali nimezaliwa mkoani Tanga kijiji cha Sangeni,Handeni ni mtoto wa pili kati ya watoto sita wa mzee Mbaruku

SWALI 2.Kitu gani kilikufanya uingie kwenye muziki?

JIBU-Wazazi walikua wanaupenda sana muziki wa dansi,haswa baba mdogo Yahaya Amir alikua chanzo cha mimi kuingia kwenye muziki wa dansi.Kwani tangu nikiwa chekechea aliona kipaji changu na kunielekeza mambo mbalimbali kuhusu muziki huu wa dansi.

SWALI 3. Katika safari yako ya muziki ni bendi gani ulizowahi kupitia?

JIBU-Nimepitia bendi zifuatazo  Watangatanga no 2,Tanga Muzika iliyokua inapiga katika baa ya Loliondo Gate,SOT Sound ambapo nilikutana Charles Baba na Waziri Sonyo bendi zote hizo za mkoani Tanga,Kisha nikajiunga Twanga Pepeta nilidumu kwa miezi mitatu nikahama na kujiunga na TOT Plus inayomilikiwa na chama cha mapinduzi ambapo nipo mpaka sasa,pia nilipita kwa kipindi kifupi katika bendi ya Rungwe.

SWALI 4.Unafahamika kama rapa hodari je kuna nafasi nyingine unaiweza kuimudu ndani ya bendi tofauti na kurap?

JIBU-Ninauwezo wa kurap, kuimba,kupiga tumba,kucheza na kutunga, lakini pia kama ujuavyo kundi letu la TOT Plus linajumuisha burudani mbalimbali,kwa hiyo mbali na bendi pia hushiriki kucheza sarakasi,kuandika miswada ya filamu,karate na boxing na vyote hivyo navifanya kwa ufanisi sibahatishi.

Hapa Juakali akicheza jukwaani

SWALI 5.Wewe binafsi umekipokeaje kifo cha kapteni John Komba?

JIBU-Nilihuzunika sana nilipopata taarifa za kifo chake kwani John Komba alikua mkurugenzi  wa aina yake katika kundi letu la TOT kifo chake kwa kweli ni pengo kubwa sio tu kwa Chama Cha Mapinduzi, familia yake na kundi letu la TOT bali ni pengo kwa Taifa zima la Tanzania,Afrika na Dunia kwa ujumla kwa mhamasishaji wa amani, upendo,utulivu na mshikamano na hata uwe na mwili almasi au dhahabu huwezi ziba pengo hili.

SWALI 6.Mwanamuziki gani wa dansi unayemkubali kati ya wale uliowahi kufanya nao kazi na kwa nini?


JIBU-Ni Ramadhani Masanja maarufu kwa jina la Banza Stone,mbali ya mapungufu ya kibinadamu,Banza Stone anajituma,ni mbunifu,ana mapenzi ya kweli kwa wenzake na kweli ni mwalimu kwa maana anaujua muziki kwa kuusomea na hana uchoyo katika kumuelekeza mtu yoyote juu ya jambo ambalo halijui.

Banza Stone 

SWALI 7.Katika kundi la TOT zimepita zama tofauti za uongozi kama vile Banza Stone,Hussein Jumbe,Badi Bakule,Muumin Mwinjuma na Ally Choki,je ni kipindi kipi kilikua na mafanikio zaidi?

JIBU- Kwa bahati mbaya sikufanya kazi na Banza Stone katika kundi la TOT,nilifanya nae kazi katika Bendi ya African Stars-Twanga Pepeta na Rungwe Band,kiukweli katika vipindi nilivyokuwepo TOT uongozi wa Badi Bakule ulikua na mafanikio makubwa kama utakumbuka albam ya MNYONGE MNYONGENI tukiwa na Panduka,Misambano, Pauline Zongo,Musa Karenga nk ilifanya vizuri mno,ila wakati sipo(wakati wa uongozi wa Banza Stone)ulifanya vizuri zaidi.


SWALI 8.Ilikuaje ukaingia Rungwe Bendi wakati ni muajiriwa wa TOT?

JIBU-Nashukuru kwamba wakati wa uongozi wa Kapteni Komba alikua akituruhusu kufanya kazi nje ya kundi pale ambapo shughuli za chama zinakua zimepungua ili mradi tu utoe taarifa kwa uongozi na sharti kubwa lilikua saa yoyote utakapohitajika unatakiwa uache hiyo shughuli mara moja na kuripoti kazini.

Juakali na Red Scorpion wakisakata dansi

SWALI 9.Unaonaje muziki wa dansi kwa sasa umepanda au umeshuka?

JIBU-Muziki wa dansi ulikua umeshuka ila kwa sasa unapanda,vyombo vya habari vinaufanya muziki upande au ushuke kwa nyakati tofauti.

SWALI 10.Bendi gani ambayo inafanya vizuri kwa sasa na kwa nini?

JIBU-Ni Bendi ya FM Academia “Wazee wa Ngwasuma” kwa sababu haitetereki kutokana na mabadiliko mbalimbali,wana nidhamu jukwaani na nje ya jukwaa,wana kikosi kilichodumu kwa muda mrefu na uongozi imara wa Nyoshi El Sadat.

Kiongozi wa Bendi ya FM Academia
Nyoshi El Sadat

SWALI 11.Vipi kuhusu familia umeoa?

JIBU-Anacheka kidogo,Kila mwanadamu anapofikia umri wa utu uzima inampasa kufanya hivyo kwa mujibu wa maagizo ya Mwenyezi Mungu na mila na desturi,kwa sasa bado sipo mbali sana itakapofika nitakujulisha inshallah.

SWALI 12.Nini Ushauri wako kwa Wanamuziki Wenzako?

JIBU-Wathubutu kujaribu kushindwa kuliko kushindwa kujaribu,wasife moyo waendelee kupambana hadi nukta ya mwisho na matokeo bora yatapatikana na wasiidhalau sifuri ndio mwanzo wa hesabu.

Kavasha inakushukuru sana Jua Kali kwa kuonyesha ushirikiano

JUA KALI anapatikana kwa namba hii ya simu +255658773737
Email au Barua Pepe:salibavicjuakali@yahoo.com


 

0 comments:

Post a Comment